MAITI ya Janeth Bambalawe(65)iliyozikwa kimamosa Usangi,Mwanga,mkoani Kilimanjaro,imerejeshwa jijini Dar Es Salaam na kuzikwa Yombo jana katika makaburi ya Kipunguni Mashariki.
Mwili wa Janeth ambao ulizikwa kwa taratibu za dini ya Kiislamu mkoani Kilimanjaro,ulipowasili jijijini Dar Es Salaam jana uliagwa na familia kwa misa ya Kikristo na baadaye kuzikwa kwa mujibu wa imani ya dini hiyo.
Ndugu wa marehemu Janeth walibaini kutokuwapo kwa maiti ya ndugu yao huyo baada ya kufika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH)kwa ajili ya kuuchukua mwili,lakini waliukosa na ndipo ilipobainika maiti yao ilichukuliwa kimakosa na familia nyingine(ya Amina Msangi)na kwenda kuzikwa Usangi.
Uongozi wa Hospitali ya Muhimbili kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi,juzi walilazimika kusafiri hadi mkoani Kilimanjaro na kuamua kuifukua maiti ya Janeth na kuirejesha Dar Es Salaam ili ikabidhiwe kwa ndugu zake.
Wakati ikifukuliwa,maiti hiyo tayari ilikuwa imekwisha kufukiwa na kukaa kaburini siku tatu,lakini katika hali ya kushangaza mwili huo ulikutwa katika hali nzuri na kurejeshwa Jijini Dar Es Salaam.
Marehemu Janeth aliugua na kufikishwa hospitalini hapo April 4,akitokea hospitali ya Amana na kulazwa wodi namba 2 Mwaisela na marehemu Amina(76),alifikishwa hospitalini hapo April 6 akitokea hospitali ya Temeke na kulazwa wodi namba 12 Kibasila,lakini wote walifariki dunia Aprili 8 na kuhifadhiwa katika Jokofu moja.
Akizungumzia tukio hilo msemaji wa familia hiyo,Peter Mkude,alisema familia imeingia gharama kwa kuendesha msiba kwa siku tatu zaidi,wakati wakisubiri maiti kurejeshwa jijini Dar Es Salaam.
Hata hivyo,alisema jana walipokea mwili wa marehemu,majira ya saa 3 asubuhi ukiwa katika hali nzuri na baadaye kwenda kuuzika kwa taratibu za Kikristo.
Kutokana na tukio hilo,Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Shirikishi wa MNH,Dk.Praxeda Ogwenyo,alisema Hospitali ya Muhimbili italipa gharama za msiba huo pamoja na usumbufu kwa familia yake.
“Hospitali italipa gharama zilizotumiwa na familia kwa siku tatu kuanzia Jumatatu hadi Jumatano.Tumewaomba watuletee risiti kama zipo,kwasababu hatuwezi kuwalipa hivi hivi,lazima tukamilishe taratibu,”alisema na kuongeza:
“Tumelazimika kuwalipa fidia kwa sababu suala hili ni nyeti na limeiweka familia katika kipindi kigumu sana,”alisema Dk.Ogwenyo.
Dk.Ogwenyo alisema waliwatuma wafanyakazi watatu kwenda kuichukua maiti iliyozikwa kimakosa na kwamba wafanyakazi hao walilipwa gharama za kujikimu ( Per diem) na gharama za mafuta za gari la kubebea wagonjwa.
“Hao wafanyakazi walilipwa per diem Sh.300,000 kila mmoja,mafuta ya gari Sh.240,000 na fedha za tahadhari Sh.200,000,”alisema Dk.Ogwenyo.
Mume wa marehemu.
Akizungumzia tukio hilo,mume wa marehemu Janeth,Theodore Chivumile (69),alisema hatalisahau tukio hilo,kwani lilimfanya akose amani kwa muda mrefu hadi walipouona mwili wa mkewe,kisha kuuzika.
Chivumile ambaye ameishi na mkewe kwa miaka 40,alisema kitendo cha mkewe kuzikwa na kukaa kaburini siku tatu na kisha kufukuliwa,kimezidisha machungu katika familia yake.
“ Muhimbili wanapaswa kujifunza kwa sababu hii si mara ya kwanza tukio kama hilo kutokea.Kwakweli linaleta simanzi sana,”alisema na kuongeza kuwa,mkewe ameacha watoto wanne na mjukuu mmoja.